![](https://lh3.googleusercontent.com/blogger_img_proxy/AEn0k_tASU6TQJ1IqJ58eHaHUbSMmaC-I2HZU6k3vsViipdvTzrVNcjfoqvG8aZ4VuR4YU8aLK7V92SomEIEqZlPTcg6HkomSU0uKo7zka6hwFnztEYtVWGVKkvZzJyDTCRyWYHa9cKsPryIhWo0174UH4rfFzsL_YWdiOEA5DpOP3S8drb_PQ73NW65dAsa5hY4KkuZ6tt1aTebCC3v9Kl6RCvMwEZPPMIQy-nn8YzF=s0-d)
YADAIWA NI KISASI CHA MAPENZI, MTUHUMIWA ATIWA MBARONI, DK BILAL AONGOZA WAOMBOLEZAJI DAR
Waandishi Wetu
MWELEKEO wa upelelezi wa mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza, Liberatus Barlow umebadilika na sasa tukio hilo linahusishwa na
kisasi cha mapenzi na tayari mtu mmoja anayedaiwa kuwa na uhusiano wa
kimapenzi Mwalimu Dorothy Moses kutiwa mbaroni na polisi.Awali, ilidaiwa
kwamba Kamanda Barlow ambaye aliuawa kwa risasi usiku wa kuamkia
Jumamosi muda mfupi baada ya kumfikisha mwalimu huyo nyumbani kwake,
alivamiwa na majambazi.
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI, Robert Manumba alithibitisha jana
kukamatwa kwa mtu huyo (jina tulihifadhi) akisema: “Ni kweli mtu mmoja
amekamatwa, lakini kwa sasa siwezi kuzungumzia kwa kina kuhusu suala
hilo kwa sababu bado tunamhoji na tunaendelea na uchunguzi.
Tutakapokamilisha, tutatoa taarifa.”
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola pia alithibitisha
kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo. Hata hivyo, alisema amesikia habari hizo
kwa kuwa yuko safarini kwenda mkoani Kilimanjaro kwenye mazishi ya
kamanda huyo... “Hayo nimesikia, lakini kwa sasa sipo Mwanza hivyo
siwezi kuzungumzia lolote.”
Habari za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, zinaeleza kwamba
upelelezi wa mauaji hayo umefanikiwa kwa hatua kubwa na kwamba mtu huyo
alikamatwa Dar es Salaam baada ya kuwekewa mtego na makachero waliopo
katika timu ya uchunguzi na alisafirishwa hadi Mwanza ambako
anashikiliwa na jeshi hilo.
Ilielezwa kuwa mtu huyo alikamatwa kutokana na kuwapo kwa taarifa za siri za kiitelejensia kutoka kwa watu mbalimbali.
“Kuna hali imefunguka na imesaidia sana. Inaonyesha kwamba Dorothy
alikuwa na uhusiano na mtu huyu ambaye alikuwa akifika nyumbani kwake,
kama mumewe na watu wanajua jambo hili,” alieleza mmoja wa askari polisi
ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Alisema kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba uamuzi wa mwalimu
huyo kusitisha uhusiano wa mapenzi na mtu huyo huenda ndicho chanzo cha
mauaji hayo lengo likiwa ni kumshawishi Dorothy kurejesha uhusiano.
“Mimi natambua kwamba huyu jamaa na Dorothy walikuwa na uhusiano na
inajulikana mjini kuwa hata mke wa mtuhumiwa anatambua jambo hilo kwani
walishagombana siku moja mjini na hata katika msiba nyumbani kwao na
mtuhumiwa,” alisema mama mmoja (jina tunalo), aliyejitambulisha kama
mmoja wa marafiki wa karibu wa Dorothy.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitangiri (jina tunalo), anasema
amekuwa akimfahamu mtuhumiwa aliyekamatwa kama baba mwenye nyumba hiyo
na kila mara amekuwa akimkuta hapo nyumbani wakati wa kujisomea na
wanafunzi wenzake.
“Mimi ninamfahamu kama baba wa rafiki yangu na nimewahi kumkuta wakati wa kujisomea hapo nyumbani na watoto wa nyumba hiyo.”
Dorothy ambaye ametajwa kuwa mjane, ni Mwalimu katika Shule ya Msingi
Nyamagana na tangu kufariki kwa mumewe Ofisa wa zamani wa TRA, Modest
Lyimo mwaka 1997.
“Watu wote wanajua kwamba mtuhumiwa alikuwa akitembea na huyo
mwalimu, wameonekana mara nyingi wakiwa muziki,” alieleza mmoja wa ndugu
wa karibu wa mke wa mtuhumiwa.
Hili ni tukio la tatu mkoani Mwanza kutokea kwa ofisa wa polisi
kuuawa. Katika tukio la awali lililotokea mwaka 1987, askari
aliyetambulika kwa jina la Inspekta Gamba aliuawa kwa risasi na watu
wanaosadikiwa kuwa ni majambazi eneo la Nyakato na katika tukio la pili
mwaka 1997, aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Kati ASP Mahende aliuawa kwa
kupigwa risasi eneo la Bugando saa nne usiku alipokuwa akifuatilia
majambazi waliokuwa wakijitayarisha kuvamia.
Dar wamuaga Kamanda Barlow
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib
Bilal aliongoza waombolezaji waliofika kutoa heshima za mwisho kwa mwili
wa marehemu Barlow nyumbani kwake, Ukonga Dar es Salaam jana.
Mwili wa Kamanda Barlow ambao unasafirishwa leo kwenda mkoani
Kilimanjaro kwa mazishi, uliwasili nyumbani kwake saa 6.45 kabla ya
kupelekwa katika Kanisa la Mtakatifu Agustino, Ukonga kwa ajili ya ibada
na kutoa heshima za mwisho.
Akitoa salamu za Serikali, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Pereira Silima alisema kifo cha Kamanda Barlow ni pengo kwa taifa...
“Tutahakikisha watuhumiwa wanapatikana kwa mikono yote miwili na hatua
za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.”
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema alisema juhudi za kuwasaka watuhumiwa zinaendelea kwa ushirikianao wa wananchi.
“Kifo cha Kamanda Barlow kimeacha pengo kwani hivi sasa askari mmoja
analinda watu 1,300 hivyo kwa kifo chake unaweza kuona ni pengo la aina
gani na ukilinganisha yeye alikuwa kamanda wa mkoa mzima,” alisema IGP
Mwema.
Alisema jeshi lake litaendelea kulinda amani ya wananchi na kifo cha Kamanda Barlow kinalifanya liongeze nguvu.
Akitoa mahubiri, Padri Veri Urio alisema kila jambo hutokea kwa wakati
na kifo cha Kamanda Barlow kimesababishwa na watu. Alisema mwenye
mamlaka ya kuondoa uhai wa mtu ni Mungu pekee hivyo waliosababisha kifo
chake siku ikifika, watajibu kwa nini walifanya hivyo.
IGP Mstaafu, Omary Mahita alisema atamkumbuka Kamanda Barlow kwa
uchapaji wake kazi tangu akiwa polisi Interpol (polisi
kimataifa)alifanya kazi kwa weledi uliotukuka.
“Daima nitamkumbuka
kwani nimefanya naye kazi sehemu tofauti na askari waliobaki waige mfano
wake wa uwajibikaji” alisema Mahita.
Mbali ya Dk Bilal, viongozi wengine walioshiriki katika ibada hiyo
jana ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, makamanda wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), makamanda wa polisi, viongozi wa
Serikali na vyama vya siasa na wananchi.
Imeandikwa na Frederick Katulanda, Mwanza na Ibrahim Yamola, Dar.
Chanzo:
www.mwananchi.co.tz