MWASISI WA NCCR MAGEUZI AFARIKI DUNIA
Mwasisi wa NCCR-Mageuzi afariki dunia
JUMATATU, OCTOBA 01, 2012 04:57 NA BENJAMIN MASESE
Mwasisi wa NCCR-Mageuzi, Emmanuel Ole Sirikwa
MWASISI wa Chama cha NCCR- Mageuzi, Emmanuel Ole Sirikwa (70) amefariki
dunia katika Hospitali ya AICC, iliyopo mkoani Arusha. Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar),
Mussa Kombo Mussa, alisema Ole Sirikwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa
wa kupooza (stroke), hadi alipofariki Septemba 28, mwaka huu hospitalini
hapo.
Alisema hadi mauti yanamkuta, marehemu Ole Sirikwa alikuwa kamishna wa
NCCR Mageuzi Mkoa wa Arusha, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na mmoja
wa wajumbe wa Baraza la Wadhamini wa chama hicho.
“Marehemu Ole Sirikwa alikuwa mwasisi wa chama aliyekuwa na kadi namba 3
ya NCCR-Mageuzi, akitanguliwa na wenye kadi namba 1 na 2 ambao
wamekisaliti chama na kuhamia kwingine kutokana na misukosuko ya
kijamii.
“Chama kimempoteza mtu muhimu ambaye hakuyumba na aliendelea kubaki
ndani ya chama chake, hali iliyotufanya baadhi yetu kumuona kama mzee wa
boma la chama,” alisema Musa na kuongeza:
“Marehemu Ole Sirikwa alibaki ndani ya chama kwa sababu ya kuheshimu na
kuthamini kile alichokianzisha, huku akiamini lengo na madhumuni yake
bado hayajafikiwa, sisi tuliobaki tutaendeleza na kuyasimamia mazuri
yote ili kufikia lengo alilokusudia,” alisema.
Mussa alisema kutokana na umuhimu wa marehemu Ole Sirikwa, chama
kimeamua kuenzi uvumilivu na misimamo yake kwa kuuita ukumbi wa mikutano
uliopo makao makuu jina la Ukumbi wa Sirikwa.
Alisema mazishi yanatarajiwa kufanyika Oktoba 3, 2012 kijijini kwake
Olijilah, Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, yakiongozwa na Mwenyekiti
chama hicho taifa, James Mbatia.
Wakati huo huo, Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi, Faustine Sungura,
alisema kitendo cha vyama vingine kuzindua kaulimbiu na kuzifanyia
kampeni nchi nzima ni dalili za kuanza kupata hofu ya uchaguzi ujao.
Sungura alisema NCCR Mageuzi imejipanga kujibu kwa vitendo kwa kuibuka
na ushindi wa wabunge mwaka 2015, licha ya kutofanya operesheni wakati
huu.
“Sisi NCCR Mageuzi tumejipanga na mipango yetu ipo ndani ya chama,
tunafanya kampeni zetu kisiri, hatuhitaji maandamano na mziki mkubwa
kwenye gari, tunataraji kuwa na mavuno mazuri kuanzia 2014 hadi 2015,”
alisema.
No comments:
Post a Comment