Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimekutana na waandisihi wa habari makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam leo, ambapo wajumbe wa Kamati Kuu, Profesa Abdallah Safari na Mabere Marando, wameweka waziwazi msimamo wa chama hicho kuhusiana na mgogoro kati ya waislamu na serikali na kukamatwa kwa Sheikh Farid huko Zanzibar.

Wanasheria hao wa CHADEMA wamesema kuwa kitendo cha serikali kumnyima dhamana Sheikh Ponda ni kinyume cha katiba na kwamba Chadema kama chama kinachojiandaa kuchukua dola, hakiwezi kuvumilia kuona haki za raia zikivunjwa.

“Tunaweza kuwa miongoni mwetu, wapo watu wanaomchukia Sheikh Ponda, lakini hatuwezi kuficha ukweli kwamba Sheikh Ponda kama raia wa Jamhuri ya Muungano au mkazi wa Jamhuri hii, anayo haki ya kusikilizwa na kupewa dhamana. Makosa ambayo Sheikh Ponda ameshitakiwa yanadhaminika kwa mujibu wa sheria, hivyo ni makosa kwa serikali kufanya hila kumnyima dhamana kiongozi huyu wa kidini,” ameeleza Marando katika mkutano huo.

Marando alifika mbali zaidi kwa kusema tatizo lililopo sasa kati ya serikali na waislamu, limetokana na hatua ya serikali kuwalazimisha waislamu wote kuwa waumini wa Bakwata, chombo ambacho wengi wanakiona kinatumika kuwakandamiza.

Naye Profesa Safari alionya matumizi ya nguvu za kijeshi yanayotumiwa na serikali kwa kisingizio cha kulinda amani, huku akieleza kuwa matumizi ya kijeshi siyo suluhu ya kutatua matatizo yaliopo.

Kuhusu kukamatwa kwa Sheikh Faridi na kumzuia kwa siku tatu, wanasheria hao wamesisitiza kuwa kitendo hicho hakikubaliki.

“Kitendo cha kumkamata na kumshikiria Sheikh Faridi, huku serikali na vyombo vyake vikisema havihusiki, wakati ukweli ni kuwa alikuwa anashikiliwa na watu wa USALAMA wa TAIFA, ni uharamia mkubwa unaopaswa kulaaniwa na wote wanaolitakia mema taifa hili,” ameeleza Marando.

Kuhusu uvunjwaji wa makanisa, Profesa Safari amesema CHADEMA kimelaani hatua hiyo iliyotokana na wananchi kujichukulia sheria mkononi. Amewataka waislamu kuvuta subira.

Hata hivyo, Profesa Safari amesena matatizo yanayotokea sasa, yameletwa na CCM kutokana na hatua yao ya kuwatumia baadhi ya waislamu kupandikiza mbegu ya udini nchini.

Chanzo Chadema Blog