Tuesday, November 6, 2012

Mauaji ya Barlow: Mtuhumiwa alihudhuria mazishi, akamatwa na vielelezo

Mauaji ya Barlow: Mtuhumiwa alihudhuria mazishi, akamatwa na vielelezo



POLISI mjini Mwanza imebaini kuwa mmoja wa watuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, alikwenda kuaga mwili wa Kamanda huyo katika uwanja wa Nyamagana sambamba na wananchi wengine.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Lily Matola jana alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Abdallah Petro ‘Ndayi’ (32) mkazi wa Mjimwema mjini hapa ambaye anashikiliwa Polisi.
Kwa mujibu wa Kamanda Matola, Petro mbali na kutajwa kuhusika na mauaji hayo, pia anadaiwa kuwa na rekodi ya kufungwa miaka 30 jela katika gereza la Butimba kwa unyang’anyi wa kutumia silaha mwaka 2006.
Alitoka gerezani mwaka 2010 baada ya kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania. Petro pia imebainika pia kuwa ni mdogo wa mtuhumiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Muganyizi Peter.
Vielelezo vyakamatwa
Kamanda Matola alisema mbali na kuwa na uhusiano huo, Petro na mtuhumiwa mwingine, Abdurahim Ismail Athuman ‘Dula’ (28) mkazi wa Mkudi Ghana, pia mjini hapa, baada ya kukamatwa kwa nyakati tofauti Mjimwema na Kilimahewa mwishoni mwa wiki, waliwapeleka polisi mahali walikoficha baadhi ya mali za marehemu.
Mali wanazodaiwa kuonesha polisi ni pamoja na redio ya mawasiliano ya Polisi na funguo za gari alilotumia kamanda Barlow siku ya tukio la mauaji yake.
Kamanda Matola alisema watuhumiwa waliwapeleka polisi katika shimo la majitaka kwenye maeneo ya Nyanshana, jijini Mwanza walipokuwa wameficha vitu hivyo.
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Joseph Konyo alisema watuhumiwa baada ya kutimiza uhalifu, walitenganisha redio hiyo ya mawasiliano ili isipatikane.
“Damu ya mtu haipotei bure, hayo yote ni pamoja na Mungu mwenyewe, kwani sisi peke yetu hatuwezi, wananchi mmetusaidia sana,” alisema Kamanda Konyo.
Baada ya kuonesha polisi vitu hivyo ambavyo sasa vimechukuliwa kama vielelezo katika kesi ya mauaji ya Barlow, Kamanda Matola alisema watuhumiwa hao walipekuliwa na kukutwa pia na kadi tatu za simu za Vodacom na Airtel, simu ya mkononi, viatu vya ngozi na begi dogo.
Pia walikutwa na kofia mbili za kijeshi aina ya bereti; moja ikiwa ya Polisi na nyingine ya kampuni ya binafsi ya ulinzi, sare za kampuni ya ulinzi, mtarimbo, bisibisi, mapanga, televisheni mbili, sub-hoofer na deki.
Alisema walipohojiwa, walidai wamekuwa wakihifadhiwa na Ryoba Matiku ‘Mama Nyangi’ katika eneo la Nyakabungo Miembeni ambako mipango yote ya uhalifu imekuwa ikisukwa. Mama huyo anashikiliwa pia kwa mahojiano.
via gazeti la HabariLeo

No comments:

Post a Comment